Jumanne 6 Mei 2025 - 12:42
Je! Ni kwa Nini Jamii Inamhitajia Mwanazuoni wa dini ya Kiislamu (Talabe)?

Wanazuoni wa dini, kama madaktari wa kiroho kwenye jamii, wana nafasi ya juu zaidi katika kutekeleza ibada za kidini. Kutokana na utaalamu wao katika elimu ya dini, wao hujibu mahitaji ya kimaanawi na kimaadili ya watu. Kwa kusoma kwa kina dini na kuitafsiri kwa mujibu wa mahitaji ya kisasa, wao huwa ni kiungo kati ya maarifa ya kidini na jamii ya kisasa. Uwepo wa maulamaa pamoja na wataalamu wa nyanja nyingine huhakikisha kuwepo kwa mizani ya maisha ya kimwili na kimaanawi katika jamii.

Kwa mujibu wa  Shirika la Habari la Hawza, katika dunia ya leo ambapo kila kitu kinabadilika kwa kasi, nafasi ya maulamaa bado ni ya msingi na yenye umuhimu mkubwa. Kwa msingi huo, hapa kuna majibu kutokana na swali linalohusu “umuhimu wa uwepo wa wanazuoni wa dini katika jamii na athari yao kubwa katika ustawi wa kiroho na kimaadili kwa jamii,” ambalo linawasilishwa kama ifuatavyo:

Swali:
Wasomi na wataalamu mbalimbali huudumia jamii kila mmoja kwa nafasi yake. Je, kuna umuhimu gani wa kuwepo kwa mwanazuoni wa dini, anayejishughulisha na kusoma na kujadili masuala ya dini? Na ni athari gani anayoleta kwenye jamii?

Jibu:
Mahitaji ya jamii hayaishii tu katika mahitaji ya kimwili. Pembeni ya hayo, yapo pia mahitaji ya kiroho, kimaadili na kimaanawi. Dini, sambamba na kuitikia mahitaji ya kimwili ya mwanadamu, hujibu pia mahitaji yake ya kimaadili na kimaanawi, na wanazuoni wa dini, kama wataalamu na wahakiki wa elimu za dini, ndio viongozi na washauri wa sehemu hii ya mahitaji ya jamii.

Kama ambavyo mtu anahitaji daktari kwa ajili ya kuponya maradhi ya mwili na kulinda afya ya kimwili, vivyo hivyo afya ya roho, akili, maadili na maisha ya kimaanawi huhitaji “madaktari wa roho.” Kazi ya maulamaa ni mwendelezo wa kazi ya manabii na Maimamu: kumtengeneza mwanadamu na kuifufua nafsi. Qur'ani Tukufu inaelezea kumfufua mtu mmoja kuwa ni kama kufufua watu wote:

«وَ مَنْ أَحْیاها فَکَأَنَّما أَحْیا النَّاسَ جَمِیعاً»

“Na mwenye kumuokoa mtu na mauti (kumfufua) ni kama amewaokoa watu wote.”
(Suratul Māida, 32)(1)

Maksud ya “kufufua” mtu mmoja katika aya hii siyo kumfufua mfu kwa maana ya mwili, bali ni tendo ambalo kwa mtazamo wa watu wenye akili, huhesabiwa kuwa ni uhai. Watu wenye busara husema, "Fulani kamfufua mtu" wakimaanisha kumponya mgonjwa, kumuokoa mtu anayezama majini, au kumuokoa mateka mikononi mwa maadui. Kwa hivyo, kauli ya “kumfufua” hapa ni katika maana ya kuokoa na kuhuisha. Mwenyezi Mungu pia ametumia kauli kama hizo katika Qur’ani Tukufu, kwa mfano, kuwaongoza watu kuielekea haki ameiita kuwa ni kuwapa uhai:

«أَوَ مَنْ کانَ مَیتاً فَأَحْییناهُ وَ جَعَلْنا لَهُ نُوراً یمْشِی بِهِ فِی النَّاسِ»

(“Je, aliye kuwa maiti kisha tukamhuisha, na tukamjaalia nuru inakwenda naye mbele za watu...”)
(Suratul Anʿām, 122).(2)

Kwa hivyo, kwa mujibu wa aya hii, yule anayemuongoza aliyepotea kwenda kwenye imani, amemfufua.(3)

Chini ya mwangaza wa dini, na kwa juhudi za maulamaa, watu wenye uwezo, waadilifu, na wataalamu wanaofaa kwa jamii hutayarishwa, na huleta manufaa kwenye jamii. Hili ni jukumu kubwa, adhimu na lenye thamani kuu.

Kwa kuwa dini ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya nyakati zote, ili kuhifadhi uhai na upya wake na uendane na mazingira ya wakati, ni muhimu kundi la watu waisome dini kwa kina, waipokee kutoka katika chemchemu safi, na kwa kutegemea tafsiri za wafasiri wa Wahyi, waiwasilishe kwa njia inayolingana na mahitaji ya wakati. Huu ndio ushahidi wazi wa ulazima wa "Ijtihād" katika dini, kazi muhimu sana inayobebwa na maulamaa, juhudi ambayo haiwezi kutekelezwa ila kwa kalamu ya wale waliotumia maisha yao yote katika kuielewa dini kwa kina.

Kuelewa dini kwa kiwango cha "ijtihād" ni sehemu tu ya majukumu makubwa ya maulamaa. Katika jamii ya Kiislamu, hasa katika zama hizi, mbali na kufikia ngazi ya "ijtihād" – jambo ambalo daima limekuwa la lazima katika historia ya Uislamu – pia kuna majukumu mengine kama kuhukumu (qadhā’), kuunda mfumo wa uchumi wa Kiislamu, kuweka uhusiano na mataifa mengine ya Kiislamu kwa msingi wa mafundisho 

ya Kiislamu, pamoja na kufanya utafiti na tafakuri katika elimu za dini na zile zinazohusiana na dini kwa mujibu wa mahitaji ya jamii. Haya yote ni miongoni mwa majukumu ya lazima ya maulamaa kwa sasa.

Kutoa fatwa, kuhifadhi Qur’ani, Sunna na urithi wa Manabii ni wajibu wa wanazuoni wa dini. Hii hufanyika kutokana na maarifa sahihi ya maulamaa kuhusu Uislamu na kwa kuichota kutoka kwenye vyanzo vya asili kama Qur’ani, Sunna, akili na uongofu wa wahyi, kisha kueneza katika jamii.

Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, tumeona kutekelezwa kwa utawala wa Mwenyezi Mungu, majukumu ya maulamaa yamekuwa maradufu: kuelimisha kuhusu masuala ya kisiasa, namna ya kuiendesha jamii chini ya uongozi wa "Walī al-Faqīh", kubainisha "fiqhi ya dola", mfumo wa maadili, mfumo wa mahakama, uchumi wa Kiislamu, na mengineyo, haya yote ni majukumu nyeti ya maulamaa wa wakati huu, ambayo hayawezi kutekelezwa ila na wao.

Leo hii, jukumu kubwa kabisa lililo juu ya mabega ya maulamaa ni kuelewa Uislamu kwa usahihi na kuwafahamisha vijana, kuondoa shubuhati (shaka) na upotofu wa kifikra na kiitikadi unaoenezwa na maadui katika jamii, na pia kulinda asili ya Kiislamu ya Mapinduzi, kulinda imani na mafundisho ya dini na kuyaelezea kwa njia sahihi kulingana na mazingira ya sasa na itikadi safi ya Kiislamu.

Kwa hivyo, kazi ya maulamaa inapaswa kupimwa kwa mujibu wa majukumu yao. Kazi yenye manufaa katika jamii haiishii katika kazi za kimwili au zile tu zenye athari za kidunia, kiasi cha kuleta shaka katika nafasi ya maulamaa.

Hatujaribu kupunguza thamani ya elimu za kimaumbile na elimu ya majaribio, bali kazi ya maulamaa ni ya aina nyingine, na hukumu juu yao inapaswa kufanywa kwa kuzingatia aina ya kazi yao.

Mtazamo unaotia shaka juu ya umuhimu wa maulamaa na athari yao katika jamii, kwa kujua au kutojua, umetokana na mtazamo wa kidunia (sekula) unaohusiana na mwanadamu na jamii, ambao huyaangalia mahitaji ya jamii kwa mtazamo wa kimwili tu, huku ukiondoa dini, maadili na maisha ya kimaanawi katika uwanja wa maisha ya kijamii, mtazamo ambao umefuatwa na wamagharibi na ambao leo hii umewatia kwenye migogoro mingi.

Rejea:

[1]. Sura al-Māida, aya 32.
[2]. Sura al-Anʿām, aya 122.
[3]. Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn, Tafsīr al-Mīzān, tarjuma ya Sayyid Bāqir Musawī Hamadānī, Qum: Dār al-Nashr al-Islāmī, 1374 Hijria Shamsiyya, juzuu ya 5, uk. 519.

Chanzo:
Kituo cha Utafiti na Kujibu Shubuhati – Hawza Ilmiyya Qom.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha